ASKOFU SANGU ASISITIZA KWARESIMA IWE FURSA YA KUTENDA MEMA BILA KUJIONYESHA KWA WATU.*

 

*ASKOFU SANGU ASISITIZA KWARESIMA IWE FURSA YA KUTENDA MEMA BILA KUJIONYESHA KWA WATU.* 


Wakristo wameaswa kuacha tabia ya kufanya wema ili tu waonekane mbele za macho ya watu, bali watende kwa sifa na utukufu kwa Mungu.


Rai hiyo imetolewa leo na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, wakati akitoa mafundisho katika Misa ya Jumatano ya majivu, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.


Askofu Sangu amewataka Wakristo kutumia kipindi hiki cha kwaresima kama nafasi muhimu ya kuongeza bidii ya kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa kuwa na moyo wa sadaka, kusali, kufanya toba na kuwatendea mema wengine, ikiwemo kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali, lakini amewaonya kutofanya hivyo kwa kujionyesha ili kujipatia sifa kutoka kwa wanadamu, na badala yake iwe ni kwa sifa na utukufu wa Mungu.


Hali kadhalika, amewataka kutokuwa chanzo cha mahangaiko na mateso kwa wengine, na badala yake wawe chimbuko la faraja, Amani, furaha, uvumilivu na upendo.


 Askofu Sangu pia amerejea Ujumbe wa Kwaresima uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa mwaka huu 2025, unaowasisitiza Waamini Wakatoliki kusimama kwa uthabiti katika Imani yao.


Amewataka kuendelea kubaki katika Imani yao bila kuyumbishwa na mafundisho yanayoutafsiri Ukristo kama njia ya mafanikio ya kiuchumi na kimwili pekee, isiyokuwa na mahangaiko yoyote ya kimaisha.

Wakati huohuo, Askofu Sangu ametumia Misa hiyo ya Jumatano ya majivu kuongoza sala maalum ya kumwombea Baba Mtakatifu Fransisko ili apone haraka maradhi yanayomsumbua.


Jumatano ya Majivu ni siku ya kwanza ya Kwaresima katika kalenda ya Kikristo ambayo ni mwanzo wa kipindi cha mfungo wa siku 40 kuelekea Pasaka, ikilenga toba, maombi, na tafakari ya maisha ya kiroho.


Siku ya Jumatano ya Majivu, waumini hupakwa majivu kwenye paji la uso kwa alama ya msalaba, huku wakihimizwa kutubu na kuamini .


Majivu hayo yanawakilisha unyenyekevu na ukumbusho kwamba binadamu ni mavumbi na mavumbini atarudi (Mwanzo 3:19).

Zifuatazo ni picha mbalimbali kutokea kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo.......
































No comments

#tuandikie maoni yako.

Theme images by Storman. Powered by Blogger.