ASKOFU SANGU KUADHIMISHA MISA YA JUMATANO YA MAJIVU
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, keshokutwa Jumatano tarehe 05.03.2025, ataadhimisha Misa ya Jumatano ya majivu katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Kwa mujibu wa Katibu wa Askofu Padre Richard Makoye, Misa hiyo itaanza saa 10:00 jioni na itahudhuriwa na Mapadre, watawa pamoja na waamini kutoka maeneo mbalimbali ya Parokia ya Ngokolo.
Padre Makoye ametoa mwaliko wa pekee kwa waamini kujitokeza kwa wingi kushiriki Misa hiyo, ambayo ni muhimu pale wanapojiandaa na kuingia rasmi katika mfungo wa Kwaresima.
Ikumbukwe kuwa, Jumatano ya Majivu ni siku ya kwanza ya Kwaresima katika kalenda ya Kikristo ambayo ni mwanzo wa kipindi cha mfungo wa siku 40 kuelekea Pasaka, ikilenga toba, maombi, na tafakari ya maisha ya kiroho.
Siku ya Jumatano ya Majivu, waumini hupakwa majivu kwenye paji la uso kwa alama ya msalaba, huku wakihimizwa kutubu na kuamini Injili.
Majivu hayo yanawakilisha unyenyekevu na ukumbusho kwamba binadamu ni mavumbi na mavumbini atarudi (Mwanzo 3:19).
Redio Faraja itarusha mubashara (Live) Misa hiyo kiwemo kupitia ukurasa huu wa Facebook.Tafadhari usikose kufuatilia.

Post a Comment